
Wachezaji wa Mbeya City wakishangilia baada ya kuifunga Prisons kwenye
Uwanja wa Sokoine ambao ni kati ya viwanja vilivyofungiwa. Picha na
maktaba.
- Viwanja vilivyofungiwa ni Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi wa Tabora, Uwanja wa Jamhuri wa Dodoma, Uwanja wa Sokoine wa Mbeya, Sheikh Amri Abeid wa Arusha, Kaitaba wa Bukoba, Mkwakwani wa Tanga na Majimaji wa Songea.
BODI ya Ligi Tanzania Bara
(TPL) imevifungia viwanja saba vinavyotumika kwa ajili ya Ligi Kuu na
Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara msimu huu.
Viwanja vilivyofungiwa ni Uwanja wa Ali Hassan
Mwinyi wa Tabora, Uwanja wa Jamhuri wa Dodoma, Uwanja wa Sokoine wa
Mbeya, Sheikh Amri Abeid wa Arusha, Kaitaba wa Bukoba, Mkwakwani wa
Tanga na Majimaji wa Songea.
TPL imevifungia viwanja hivyo kutokana na matatizo
mbalimbali yakiwemo ya mapaa, majukwaa, sehemu ya vyumba vya
kubadilishia nguo na eneo la kucheza mpira wa miguu.
Bodi ya Ligi imechukua hatua hiyo wakati Ligi Kuu
Bara imesimama hadi mwishoni mwa Januari kwa hiyo kuna kipindi kirefu
hadi vitumike kwa ligi hiyo.
Ni matarajio yetu kwamba wamiliki wa viwanja hivyo
watachukua hatua thabiti katika kuvifanyia matengenezo viwanja vyao ili
viwe kwenye hali nzuri kabla ya mashindano hayo kuanza tena.
Ieleweke kwamba hakuna maendeleo ya mpira wa miguu
kama kutakuwa hakuna viwanja bora vya kuchezea kwani juhudi zote
zingine zitakazofanywa hazitazaa matunda.
Viwanja ni moja ya nyenzo muhimu katika mpira wa
miguu kwa hiyo ni muhimu kwa kila mdau kuelewa jambo hilo na wanaohusika
kulitilia mkazo kwa kuwa na viwanja bora.
Inafurahisha pia kusikia kwamba Shirikisho la Soka
la Tanzania (TFF) linaunga mkono hatua ya Bodi ya Ligi kuwa litaisaidia
ili kuhakikisha kuwa mpira wa miguu unachezwa katika viwanja bora.
Lakini, ni muhimu sana kwa TFF na Bodi ya Ligi
kuhakikishwa kwamba viwanja ambavyo havikufanyiwa marekebisho
yanayotakiwa havitumiki katika mzunguko wa pili wa ligi hizo.
Klabu za Tanzania zinapaswa kuwa na viwanja vyake,
lakini ukweli ni kwamba baadhi ya klabu hizo hazina uwezo wa kumiliki
au kujenga viwanja kwa ajili yao. Lakini, ziko klabu zenye uwezo wa kuwa
na viwanja kama vile Simba na Yanga kutokana na rasilimali kubwa
waliyonayo ikiwemo wingi wa wanachama na mashabiki wanaoziunga mkono.
Kwa hiyo, wakati umefika kwa klabu za Simba na
Yanga kuwa na viwanja vya kisasa ambavyo watavitumia kwa kucheza mechi
za nyumbani za Ligi Kuu na mechi za kirafiki.
Jambo hilo mbali na kuwapunguzia gharama za
michezo pia zitawaongezea kipato na katika uwanja huo wanaweza kutoa
ofisi na sehemu za kufanyia biashara ambazo zitawaingizia fedha nyingi.
Klabu za Simba na Yanga zina nafasi ya kuingia ubia na kampuni
kadhaa zikiwemo benki katika mradi wa ujenzi wa uwanja wa kisasa ambao
utakuwa ni kitega uchumi kikubwa.
Viongozi wa klabu hizo wanatakiwa kufungua macho
na kuziona fursa za maendeleo ya klabu zao na kuzichangamkia badala ya
kuziendesha klabu hizo kwa mtindo wa kizamani wa kutegemea mapato ya
mlangoni tu.
Mapato ya mlangoni ni muhimu lakini yakiongezeka
na vyanzo vingine vya mapato vitavijengea klabu hizo kuwa na uwezo
mkubwa wa kifedha na kuwa na uwezo wa kusajili wachezaji bora zaidi na
wakati huo wataanza kuwa na wazo la kuchukua ubingwa wa Afrika. Hakuna
sababu yoyote ile kwa sasa ambayo inazifanya Simba na Yanga na hata Azam
za Dar es Salaam kuwa zisiwe klabu kubwa na zinagombania vikombe vya
Afrika kwenye hatua za fainali kila mwaka.
No comments:
Post a Comment